Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, Rabbi Dov Lando, kiongozi wa kiroho wa mkondo wa Haredi (Wayahudi wenye msimamo mkali zaidi wa kidini, ambao sehemu kubwa ya wafuasi wao wanapinga huduma ya lazima katika jeshi la utawala wa Kizayuni) wa Degel HaTorah (moja ya vyama vya kisiasa vya Haredi na mwakilishi wa mkondo wa Kilithuania usio wa Kihasidic nchini Israel), amekosoa vikali mikondo ya Uzayuni wa Kidini na kudai kuwa vita vinavyoanzishwa na jeshi la utawala wa Kizayuni havilengi kuutetea utawala huo, bali "ni mfano wa mauaji."
Lando alisema: "Serikali, kwa jina la heshima na fahari ya nchi, inawapeleka wanajeshi vitani na wao wanawaua watu. Je, hilo pia linaruhusiwa? Hayo ni mauaji ya wazi, wanachokifanya ni kuhamasisha mauaji."
Kufuatia kauli hizo, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, alizilaani kauli za Lando na kudai kuwa wanajeshi wa kidini, wa kisekula na wa Haredi wanaohudumu katika jeshi la utawala huo wanayahatarisha maisha yao kwa ajili ya kuilinda Israel.
Netanyahu pia alidai: "Wanajeshi wa jeshi la Israel wanastahili kuthaminiwa kwa dhati, kushukuriwa na kuungwa mkono kikamilifu na makundi yote ya jamii, ikiwa ni pamoja na jamii ya kidini inayozingatia mafundisho ya Taurati."
Kujibu msimamo huo, Harakati ya Degel HaTorah ilimwonya Netanyahu kutomlenga kwa mashambulizi ya kisiasa kiongozi wake wa kiroho. Katika taarifa ya harakati hiyo ilielezwa: "Kauli za wanazuoni wakubwa na wasomi wa Taurati ni miongoni mwa mambo matakatifu zaidi kwa taifa la Israel, wale ambao hawaelewi misingi ya fikra zao hawapaswi kukimbilia kuzifasiri kauli zao au kuwashambulia, jiepusheni na cheche za moto wao."
Gazeti la Jerusalem Post pia lilikumbusha kuwa; mwanzoni mwa mwezi huu, Lando aliwaagiza wanafunzi wa Haredi kutoshirikiana kwa namna yoyote na jeshi la utawala wa Kizayuni na kupuuza kabisa hati za kuitwa kuhudumia jeshini.
Lando pia alidai kuwa hapo awali kulikuwa na makubaliano kati ya serikali na viongozi wa kidini kuhusu kuwapa wanafunzi wa Yeshiva (vyuo vya juu vya masomo ya dini ya Kiyahudi) msamaha wa huduma ya kijeshi, lakini Mahakama Kuu ya Israel ilikomesha makubaliano hayo kwa vitendo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Lando alisisitiza kuwa; Mahakama Kuu ya Israel "imetangaza vita dhidi ya jamii ya kidini inayozingatia Taurati," na akabainisha kuwa jamii ya Haredi haipaswi tena kushirikiana na jeshi la utawala wa Kizayuni, ambalo ndilo linatekeleza maamuzi ya mahakama hiyo.
Maoni yako